10 Oktoba 2025 - 14:04
Kuanza kwa kuondoka kwa majeshi ya wavamizi (wa kizayuni) kutoka Ghaza

Baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Ghaza yanashuhudia kuondoka kwa hatua kwa hatua kwa majeshi ya utawala wa Kizayuni na kuanza kwa kurejea kwa wakimbizi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kimeripoti kuwa majeshi ya utawala wa Kizayuni yameanza kuondoka hatua kwa hatua kutoka katika baadhi ya mitaa ya mji wa Ghaza, na kurejea kwa wakimbizi katika mitaa ya Al-Nasr, Al-Tuffah, na Al-Saftawi katika mji wa Ghaza kumeanza.

Mwandishi wa kituo cha habari cha Al-Hadath naye ameripoti kuwa Jeshi la 36 la Golani limeanza kuondoka kutoka Ukanda wa Ghaza.

Kituo cha runinga cha Channel 12 cha utawala wa Kizayuni kimeripoti kuwa Kikosi cha Saba cha Jeshi kimeanza kuondoka kutoka Ukanda wa Ghaza.

Tovuti ya Walla pia imenukuu vyanzo vya habari ikisema: “Majeshi ya Israel yameanza kuondoka kutoka mji wa Ghaza na kambi ya wakimbizi ya Al-Shati. Vikosi hivyo vitawekwa katika maeneo mbalimbali. Mchakato wa kuondoka ni mgumu na nyeti, na jeshi halitaki kuchukua hatari.”

Vyanzo hivyo vimeongeza kuwa: “Jeshi limepunguza idadi ya wanajeshi wanaoshiriki katika operesheni huko Ghaza, na limeviondoa vikosi vilivyokuwa chini ya Brigedi ya Golani pamoja na vikosi vingine.”

Redio ya Jeshi la utawala wa Kizayuni nayo imeripoti kuwa majeshi ya Israel yaliyoko Ghaza hivi karibuni yatakamilisha kuondoka hadi kufikia mstari wa manjano uliokubaliwa.

Kabla ya hapo, utawala wa Kizayuni ulikuwa umevunja makubaliano ya kusitisha mapigano, ambapo helikopta na mizinga ya jeshi la utawala huo ziliyashambulia maeneo ya mashariki ya mji wa Ghaza.

Aidha, shambulio la angani lilifanywa dhidi ya nyumba moja kaskazini mwa mtaa wa Al-Nasr katika mji wa Ghaza.

Vilevile, boti za kijeshi za utawala wa Kizayuni zililishambulia barabara ya Al-Rashid katikati ya Ukanda wa Ghaza.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha